ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

ZAIDI YA WANANCHI 230 WA TARAFA YA MVUMI WAPATIWA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.

05 Sep, 2024
ZAIDI YA WANANCHI 230 WA TARAFA YA MVUMI WAPATIWA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.

THBUB inafanya tathimini ya hali ya haki za binadamu na utawala bora nchini ili kuhakikisha kwamba haki hizo zinalindwa na kuhifadhiwa kama ilivyoainishwa katika   Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

Hayo yamebainishwa na Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka THBUB Bw. Said Zuberi wakati akitoa elimu kwa jamii kuhusu Haki za Binadamu, na Utawala Bora, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Chihembe kilichopo Kata ya Mvumi, Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, Septemba 4, 2024.

Bw. Zuberi ameeleza kuwa licha ya tathmini inayofanywa na tume, imekuwa ikifanya tathmini na kutoa mapendekezo kwa Serikali na wadau kuhusu uboreshaji wa haki za binadamu nchini.

‘’Ibara ya 12 (1)(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, hivyo kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake"alisema Bw. Saidi

 Pia, ameeleza kuwa wajibu wa kulinda haki za binadamu ni wa kila mtu hivyo basi, amewataka wananchi wote hasa wa Kata ya Mvumi, kutoa taarifa bila kusita kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) pale wanapokutana na matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika jamii.

 

 

Aidha, Bw. Zuberi aliongeza kuwa majukumu ya THBUB yanapatikana katika Ibara ya 130 (1)(a) - (h) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

“THBUB inajukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi; kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jamii; kufanya uchunguzi juu ya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora; kufanya utafiti, kutoa na kueneza elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora’’ alisema Bw. Zuberi.

Mkutano huo wa hadhara ni utekelezaji wa jukumu la Tume kikatiba la kuhakikisha elimu kuhusu haki za binadamu na utawala bora inatolewa nchini. Mkutano huo pia, ulihudhuriwa na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mvumi Bw. Haamisi Onesmo Chibago na viongozi mbalimbali katika ngazi ya Tarafa na Kata.