WATENDAJI WATAKIWA KUZINGATIA MISINGI YA UTAWALA BORA

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma kuzingatia misingi ya Utawala Bora katika utekelezaji wa majukumu yao. Hayo yameelezwa na Kamishna Amina Talib Ali wakati akitoa mafunzo maalum kwa watendaji wa Kata Wilayani Kibondo Februari 18, 2025.
Mhe. Amina ameelaza kuwa lengo la kuwapatia mafunzo hayo ni kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwa na Serikali inayozingatia misingi ya utawala bora nchini.
“Mpo mpakani na hapa mnaingiliana na nchi mbalimbali, ninyi ni kioo cha Tanzania kwa majirani zetu, uzingatiaji wa misingi ya Utawala Bora ni lazima hilo halina mjadala” Alisema mhe. Amina
Mhe. Amina aliongeza kuwa watendaji wanatakiwa kukumbuka kuwa suala la utawala bora linaenda sambamba na uzingatiwaji wa haki za binadamu. Kiongozi yeyote anayezingatia utawala bora ni lazima awe makini katika kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa kama zinavyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba mbalimbali tuliyoiingia ya Kimataifa na ya Kikanda.
“Sisi kama Tume tutaendelea kuwapatia elimu stahiki inayohusu masuala yaHaki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora, hii ni kazi yetu na pia ni jukumu tulilopewa kisheria na nchi”. Alisema Mhe.Amina
Kwa upande wa watendaji walipata fursa ya kuwasilisha changamoto zao ikiwa ni pamoja na mazingira yasiyo rafiki katika utendaji kazi kwani hawana usafiri na wamekuwa wakihudumia maeneo makubwa pamoja na kuingiliwa majukumu yao na viongozi wa kisiasa.