VIJANA WALIOKO VYUONI WATAKIWA KUWA WAWAKILISHI WAZURI KWA VIJANA WENZAO

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka vijana waliopo vyuoni kuwa wawakilishi wazuri kwa vijana wenzao ambao sio wanavyuo kwa kuwaelemisha kuhusiana na maswala ya haki za binadamu na utawala bora.
Wito huo umetolewa na Afisa Mafawidhi wa THBUB Tawi la Dar es salaam, Bi. Shoma Philip, alipokuwa akizungumza na Viongozi na Wanachama wa Klabu ya Haki za Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) katika Ofisi za Tume Tawi la Dar es salaam, Machi 3, 2025.
Viongozi na wanachama walifika katika Ofisi za Tume kwa lengo la kujifunza na kueleza malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu 2025.
Bi. Shoma amewataka Viongozi na wanachama hao kutumia vizuri elimu waliyoipata kuhusu haki za binadamu na utawala bora na kutakiwa kuwa wawakilishi wazuri kwa vijana wengine ambao hawapo vyuoni na hawajapata fursa kama yao ya kupata elimu kuhusiana na ukuzaji, ulinzi na utunzaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
“Haki za vijana wengi zinapotea bila ya wao wenyewe kujua na kutokana na mazingira wanayoishi, kwahiyo ninyi ni kundi linalowawakilisha vijana wengi, walioko vyuoni na pia wale ambao hawapo vyuoni, hivyo mnalo jukumu la elimu mnayoipata inawafikia vijana wenzenu ili kupunguza vitendo vya ukiukwajia wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora “.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Haki za Binadamu Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Bw. Denis F Athanaz alipata nafasi ya kuelezea mafaniko mbalimbali ambayo Klabu imeyapata tangu kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya haki za binadamu kwa wanafunzi wenzao kupitia semina, midahalo na makongamano, kuongezeka kwa wanachama hai, kukuza ushirikiano na taasisi mbalimbali pamoja na kuimarisha misingi ya utu ndani ya chuo hicho.
Wakiwa katika Ofisi za Tume viongozi na wanafunzi hao walipata fursa ya kujifunza mada ya haki za binadamu, misingi, nguzo na umuhimu wa Utawala bora. Pia walipatiwa vitendea kazi ambavyo vitawasaidia wanapokuwa wanatoa elimu ya haki za binadamu kwa vijana wenzao.
Aidha, Viongozi na Wanachama hao waliishukuru THBUB kwa juhudi zake za kuhakikisha elimu ya haki za binadamu inafika chuoni kwao, na pia walieleza malengo yao makubwa kwa mwaka huu na kuiomba Tume kuendelea kuwaunga mkono na kuendelea kushirikiana nao ili kuweza kufanikisha malengo hayo.