TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI NYINGINE KUHAKIKISHA HAKI ZA BINADAMU ZINALINDWA.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mohamed Khamis Hamad amezitaka taasisi nyingine za Serikali kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa Tume katika kutatua malalamiko ya wananchi, ili kuhakikisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora zinazingatiwa na kulindwa.
Bw. Mohamed aliyaeleza hayo wakati wa mahojiano maalum na kituo cha redio cha CG FM Mkoani Tabora leo alipo kuwa akijibu swali la mwandishi la namna THBUB inavyoshirikiana na Taasisi nyingine za Serikali katika kuhakikisha haki za Binadamu na Utawala Bora zinazingatiwa.
”Tumekuwa na mawasiliano mazuri na baadhi ya Taasisi za Serikali hivyo inapotokea wananchi wameleta malalamiko THBUB huwasiliana na Taasisi husika na kuhakikisha inafuatilia ili kuhakikisha haki inapatikana.
Bw. Mohamed alisema kuna
baadhi ya wananchi wana malalamiko ya msingi kabisa lakini hawajiu mahali pa kupeleka hayo malalamiko. Jukumu la Tume ni kupokea malalamiko hayo na kuyapeleka katika Taasisi husika na kufuatilia mpaka mwisho wa lalamiko hilo.
Amesisitiza kwa Taasisi za Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha pale wanapopelekewa hoja za kushughulikia kwa kuwa nia ya Serikali yeyote duniani ni kufanya kazi kwa niaba ya wananchi walio wengi.
Akiongelea hali ya Haki za binadamu nchini alisema kwa sasa kuna maendeleo makubwa ya haki za binadamu nchini kwakuwa Wananchi wengi wameanza kufahamu haki zao ni zipi, uhuru wa kutoa maoni umeongezeka, haki ya kisiasa pia imeimarishwa kwa uwepo wa vyama vingi vya siasa.
Aidha alisema kampeni mbalimbali zimeanzishwa kama kampeni ya Mama Samia Msaada wa Kisheria, ila pia idadi ya matukio yanayoripotiwa ya uvunjwaji wa haki za binadamu yameongezeka.
Hata hivyo alisema zipo changamoto pia, kwani hakuna nchi yeyote duniani ambayo ina haki za binadamu kwa asilimia mia moja ili kuweza kupunguza changamoto zilizopo. THBUB itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuongeza uelewa.