ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YATOA TAMKO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

09 Mar, 2023
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YATOA TAMKO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzana (THBUB) ,imeungana na jamii na wadau mbalimbali duniani kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwa kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake duniani.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka 2023 ni “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu Katika Kuleta Usawa wa Kijinsia.” Kauli mbiu hii inakumbusha umuhimu wa ujumuishi wa wanawake katika masuala ya teknolojia na kutafakari juu ya namna teknolojia inavyoweza kuwa kichocheo au kizuizi cha kujiletea usawa wa kijinsia.
 

Akitoa tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani jijini Dodoma leo Machi 8, 2023 Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe.Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema kuwa kupitia kauli mbiu hiyo tume inapata fursa ya kujadili na kuandaa mikakati madhubuti itakayosaidia kutumia teknolojia na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na makundi mengine yenye mahitaji maalum, zikiwemo zile zinazotokana na teknolojia yenyewe katika kutokomeza ukatili na kuleta usawa wa kijinsia.
 

"THBUB inatambua kuwa teknolojia ikitumika vyema inakuwa chachu kwa maendeleo ya wanawake na Taifa kwa ujumla; Lakini ikitumika vibaya inaweza kuchangia uvunjifu wa haki za binadamu. Katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia duniani, kumekuwepo na changamoto za matumizi ya teknolojia ambapo wakati mwingine imechangia ukatili wa kijinsia,"
 

"Mathalani, baadhi ya watu, hasa wapenzi kutumia simu na vifaa vingine vya kielektroniki kujirekodi wakiwa katika faragha lakini pale inapotokea kutoelewana picha hizo zimekuwa zikirushwa mitandaoni kwa lengo la kudhalilisha ambapo wahanga wengi wa matukio haya wamekuwa ni wanawake na watoto. Aidha, kumekuwepo maendeleo hafifu ya matumizi ya teknolojia katika maeneo ya vijijini tofauti na mijini," amesema Mwaimu

Mhe.Mwaimu ameitaka jamii kuhamasika katika kuendelea kutumia teknolojia kwa weledi, kwa kuzingatia sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Pia ametoa wito kwa wanawake kuendelea kujiamini na kutumia teknolojia katika kujiletea maendeleo yao kiuchumi na kijamii na kuiomba Serikali na wadau mbalimbali kuandaa programu maalum kuwasaidia wanawake hasa wa vijijini kutumia teknolojia katika kujikwamua kiuchumi na kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Tarehe 8 Machi kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya kutambua utu, nafasi na mchango wa mwanamke katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa duniani. Umoja wa Mataifa uliridhia na kuanza kuadhimisha rasmi siku ya wanawake Duniani, Machi 8 mwaka 1975 kwa lengo la kuikumbusha dunia juu ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Uamuzi huu ulifikiwa ili kupinga mfumo dume ambao ulizikabili jamii mbalimbali duniani na kuminya haki za wanawake kama miongoni mwa makundi maalum.