ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA KUTOA ELIMU KWA WAKAZI NA WANAFUNZI IRINGA

18 Feb, 2025
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA KUTOA ELIMU KWA WAKAZI NA WANAFUNZI IRINGA


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Dkt. Thomas Masanja amesema THBUB inatarajia kutoa elimu kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Wakazi na Wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwawezesha kutambua haki zao na kudumisha utawala unaozingatia haki za binadamu.

Mhe. Dkt. Masanja ameyasema hayo leo Februari 17, 2025, wakati THBUB ilipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Elia Lupanda kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea namna zoezi hilo la kutoa elimu litafanyika.

Amesema Tume itatoa elimu kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kupitia mikutano ya hadhara, itapokea malalamiko yanayohusu haki za binadamu na utawala bora kwenye maeneo yao, na pia Tume itawafikia wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo vilivyopo mkoani humo.

Aidha, zoezi hilo litaambatana na kutembelea Magereza za Mkoa huo kwa lengo kukagua na kutathmini haki za watu wanaozuiliwa, na kutoa mapendekezo jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo kwa mujibu wa taratibu na Sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kukagua viwango vya kimataifa na kikanda vinavyolinda na kutetea haki za binadamu ikiwemo makundi ya watu waliozuiliwa.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Bw. Elia Lupanda ameipongeza na kuishukuru THBUB kwa kufika Mkoani Iringa na kupitia elimu hiyo Wananchi wake watazitambua haki zao na kukuza misingi ya utawala bora