ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAZINDUA RASMI KLUB YA HAKI ZA BINADAMU KATIKA CHUO KIKUU CHA IRINGA 

23 Feb, 2025
THBUB YAZINDUA RASMI KLUB YA HAKI ZA BINADAMU KATIKA CHUO KIKUU CHA IRINGA 

Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ukiongozwa na Kamishna Mhe.Dkt. Thomas Masanja umezindua Klabu ya haki za binadamu katika Chuo Kikuu cha Iringa, leo Februari 20, 2025.

Uzinduzi huo umefanyika wakati ujumbe huo ulipofika Chuoni hapo kwa lengo la kutoa elimu ya kusimamia na kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dkt. Masanja ameshukuru Chuo hicho kwa mapokezi mazuri na kupongeza jitihada zilizofanywa na Klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023,

“Kwanza kabisa niwashukuru kwa kutupokea, pili niwapongeze kwa historia nzuri tuliyoisikia, Klabu ilianza mwaka 2023 lakini pamoja na uchanga wenu mmeweza kufanya vitu vingi sana, kwahiyo nichukue nafasi hii kwa niaba ya THBUB kuwapongeza sana “ amesema Dkt Masanja.

Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa Prof. Mathias .G. Sahinkuye ameishukuru THBUB kwa uwepo wao na kuendelea kujitoa kukuza haki za binadamu na utawala bora katika nchi yetu ya Tanzania.

Aidha, kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu ya Haki za Binadamu Chuoni hapo Bw. Richard Mokily ameeleza shughuli mbalimbali ambazo klabu hiyo imeweza kuzifanya tangu kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja na kushiriki vikao na semina mbalimbali za kuwajengea uwezo Viongozi katika masuala ya haki za binadamu, kukamilisha usajili wa klabu, kushiriki Maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Haki za Binadamu Ulimwenguni na pia kutoa misaada kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji.