THBUB YATOA RAI KWA WANANCHI WA KATA YA ILEMBULA MKOANI NJOMBE

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Dkt. Thomas Masanja ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Aprili 2, 2025 katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ilembula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoani Njombe Dkt. Masanja alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi binafsi na wananchi katika kukuza na kulinda haki za kiraia na kisiasa pamoja na haki za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kama zilivyoainishwa katika Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.
Dkt. Masanja alieleza kuwa THBUB imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha haki za kila Mtanzania zinalindwa na kukuzwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Sheria za nchi.
“THBUB ipo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa haki za kila mtanzania zinakuzwa na kulindwa na tumejipanga kushirikiana na wadau wote mkiwemo wananchi ili kuhakikisha kila mtu anapata haki zake bila ubaguzi wowote “amesema Dkt. Masanja
Aidha, Dkt. Masanja alihimiza wananchi kutoa taarifa juu ya vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya madaraka na ubaguzi wa aina yoyote.
Aidha, Wananchi wa Kata ya Ilembula walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na haki za binadamu na utawala bora ambapo wengi wao walipongeza juhudi za THBUB katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa utawala wa sheria na uwajibikaji wa viongozi