THBUB YATOA ELIMU KATIKA VYUO VYA MAFUNZO YA AMALI, PEMBA
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa elimu ya haki za binadamu na Utawala Bora katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mtambike kilichopo katika Wilaya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, na Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya na Shule ya Msingi Daya vilivyopo Vitongoji, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Afisa Uchunguzi Mkuu Bw. Ramadhan Slaa alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kuanzisha Klabu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya THBUB na taasisi za elimu nchini ili kuwa na kizazi chenye kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia misingi ya utawala bora.
Aidha, Bw. Ramadhan Slaa amewaasa wanafunzi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa jamii zao katika kueneza dhana halisi ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuwa na jamii yenye uelewa mpana kwa maeneo hayo.
Katika hatua nyengine, Bw. Slaa alimshauri Mkuu wa Chuo cha Daya kilichopo Mtambwe, Mwl. Saada Ali Hamad, kuanzisha na kuimarisha Klabu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chuoni hapo ili kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu kwa walimu na wanafunzi na hivyo kuwa na jamii yenye kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Adha, Mwalimu wa Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Vitongoji na Mkuu wa Idara ya Masomo Mtambukwa chuoni hapo, Bw. Khamis Abdalla Khamis aliishukuru THBUB kwa kutembelea chuoni hapo pamoja na kuishauri THBUB kuwa karibu na Klabu hizo ili kuziimarisha na kuzifanya ziwe endelevu. Pia, aliahidi kuzisimamia vyema katika kuendeleza shughuli za kutoa elimu kupitia klabu hizo.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti wanafunzi wa vyuo hivyo, walipata fursa ya kuuliza maswali kuhusiana na Dhana, Chimbuko na Umuhimu wa Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora, na umuhimu na faida za kujiunga na Klabu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Vile vile, wanafunzi hao waliiomba THBUB kufanya ziara za mara kwa mara katika vyuo hivyo vyuo kwa ajili ya kutoa elimu.
Katika mafunzo hayo, jumla ya wanafunzi 600 wakiwemo wanafunzi 400 kutoka Chuo Cha mafunzo ya Amali cha Vitongoji na wanafunzi 200 kutoka chuo cha Daya, Mtambile walishiriki. Mafunzo hayo yalisaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora na umuhimu wa kujiunga na Klabu ya Haki za Binadamu katika vyuo hivyo na jamii kwa ujumla.