THBUB YASISITIZA ULINZI WA HAKI ZA WAANDISHI WA HABARI.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Nyanda Shuli asisitiza ulinzi wa haki za waandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Waandishi wa habari wanapokumbana na misukosuko wakiwa kazini, ni jukumu letu kama taasisi za haki za binadamu kusimama nao na kuhakikisha haki zao zinalindwa,” amesema Mhe. Shuli.
Mhe. Shuli amesema hayo katika kikao cha wadau wa tasnia ya habari kilichofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 29, 2025 kikiwa na mada kuu “Empowering Journalists for Informed Communities in Tanzania”
Mgeni rasmi katika kikao hicho, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura, aliwahakikishia wadau wa habari kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kwa lengo la kuweka mazingira salama kwa waandishi kutekeleza majukumu yao.
“Vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kujenga jamii yenye uelewa. Ushirikiano kati ya waandishi na vyombo vya dola ni jambo la lazima ili kulinda amani na kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinasaidia maendeleo ya nchi,” amesema IGP Wambura.
Aidha, Mhe. Shuli aliwasilisha uzoefu wa THBUB katika kutetea waandishi wa habari wanaokumbana na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kusisitiza kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa mpana na inayoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa
Kikao hicho kimeandaliwa na IMS, Jamii Africa na UTPC kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania.