THBUB YAPOKEA MALALAMIKO YA WANANCHI KIGOMA

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa mkoa wa Kigoma.
Malalamiko hayo yamewasilishwa na wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora uliofanyika katika Mtaa wa Kamala, kata ya Bangwe, Manispaa ya Kigoma Februari 10, 2025.
Akizungumza mara baada ya kupokea malalamiko hayo Kamishna wa THBUB Mhe. Amina Talib Ali amesema kuwa, kwa utaratibu, Tume inatoa siku tisini kupata mrejesho wa malalamiko yanayowasilishwa mbele yake. Hivyo, kuahidi kuyafanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa mbele ya Tume katika Mkutano huo na kutoa mapendekezo kwa Serikali.
Ziara ya Ujumbe wa THBUB Mkoani Kigoma ina lengo la kuitambulisha Tume, kutoa elimu ya Haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kupokea malalamiko.
THBUB inalenga kuzifikia Wilaya za Buhigwe, Kakonko, Kibondo, Kigoma Manispaa na Wilaya ya Kigoma.