ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB yalaani mauaji ya Bw.Ally Kibao kiongozi wa CHADEMA

12 Sep, 2024
THBUB yalaani mauaji ya Bw.Ally Kibao kiongozi wa CHADEMA

Tume ya haki za binadamu na utawala bora THBUB imelaani vikali mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Bw. Ally Mohammed Kibao aliyeuwawa na watu wasiojulikana na kutupwa eneo la Ununio Jijini Dar es salaam.

Hayo yamebainishwa Septemba 9,2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo.

Mhe. Mwaimu amesema kuwa kitendo hicho kinakiuka haki za msingi zilizo katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa katika ibara ya 14, ukatili dhidi ya binadamu ambayo ni kinyume na ibara ya 13(6)(e) na ukiukwaji wa haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru iliyotamkwa katika ibara ya 15(1)(2).

“Kitendo alichofanyiwa Bw,Kibao ni ukatili usio faa katika Jamii yetu,ni wajibu wa kila mtu kuheshimu  haki za binadamu na kulinda utu wa mtu”amesema Mhe.Mwaimu

Aidha,Mhe. Mwaimu amefafanua kuwa THBUB inaendelea na kazi ya kufuatilia matukio kama haya yanayoendelea nchini ikiwa ni pamoja na hili.
“Hivyo nitoe wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa THBUB na vyombo vingine vya dola vinavyochunguza matukio hayo “. Amesema Mhe. Mwaimu

Kwa hatua nyingine Mhe.Mwaimu amesema kuwa THBUB inatambua maelekezo ya Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa vyombo vya uchunguzi kufuatilia na kuwasilisha taarifa za kina kuhusu tukio hilo la kikatili na mengine ya namna hii yanayoendelea kutokea nchini.

Pia Mhe.Mwaimu alito wito kwa wananchi wote kuendelea kuwa watulivu na wenye Subira wakati  vyombo vya dola vinaendelea na kazi ya uchunguzi.

Mwisho THBUB inatoa pole kwa Viongozi na Wanachama wa CHADEMA,familia,Ndugu,Jamaa na marafiki wa Bw.Ally Kibao kwa msiba mzito wa kupoteza mpendwa wao.