ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Urusi

22 Jan, 2024
THBUB kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Urusi

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ya Tanzania na Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya nchini Urusi (Office of the High Commissioner for Human Rights in the Russian Federation) leo Januari 20, 2024 zimetiliana saini makubaliano ya mashirikiano (MoU) katika kukuza na kulinda haki za binadamu katika mataifa yao.

Utilianaji saini makubaliano hayo umefanyika Ofisi Kuu ya THBUB Kilimani, Jijini Dodoma mbele ya vyombo vya habari, huku viongozi wa ngazi za juu wa taasisi hizo mbili wakishuhudia tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mst.) taasisi hizo zitashirikiana katika masuala ya mafunzo, kufanya tafiti, na kuandaa semina na makongamano ya kisayansi yanayolenga kuboresha mifumo ya shughuli za haki za binadamu katika ngazi za kitaifa na kikanda.

Pia, taasisi hizo zitafanya ziara na mikutano baina yao ili kubadilishana uzoefu, Mhe. Mwaimu alisema.

Katika hafla hiyo ya utilianaji saini makubaliano ya mashirikiano Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohamed Khamis Hamad; Wahe. Makamishna wa Tume, Dkt. Thomas Masanja na Nyanda Shuli; na Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Patience Ntwina.

Wakati ujumbe wa Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya nchini Urusi uliongozwa na Naibu Mkuu wa Utawala, Bwana Ilya Chechelnitskii akiambatana na Mkuu wa Idara ya masuala ya Kimataifa, Bwana Viacheslav Tolmachev; Mtaalam wa masuala ya Kimataifa, Bwana Grigorii Malinkin; na Mkuu wa masuala ya Habari, Bi. Tatiana Dzhedzhula.