THBUB KUSHIRIKIANA NA AFRICA COURT COALITION.

Katika kukuza na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepanga kuendeleza mashirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 11 Julai 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mohamed Khamis katika kikao kilichofanyika kati ya THBUB na ujumbe kutoka Africa Court Coalition katika ofisi za Makao Makuu ya THBUB-Dodoma.
Mhe.Mohamed ameipongeza taasisi ya Africa Court Coalition pamoja umoja wa mawakili wa Afrika Mashariki kwa kazi kubwa wanayoifanya, hususan katika kuhakikisha kuwa amri zinazotolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu zinatekelezwa.
Mhe.Mohamed ameeleza zaidi kuwa ushirikiano baina ya THBUB na taasisi hiyo utaleta tija katika kuishauri serikali katika kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu.
Aidha, kwa upande wake mratibu wa taasisi hiyo Bi.Sofia Ebby ameishukuru THBUB kwa kukubali mashirikiano hayo yatakayosaidia kuimarisha masuala mbalimbali ya utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.