ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB IPO KWA AJILI YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KERO ZINAZOHUSIANA NA HAKI ZA BINADAMU

14 Mar, 2025
THBUB IPO KWA AJILI YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KERO ZINAZOHUSIANA NA HAKI ZA BINADAMU

Wananchi wa Kijiji cha Lulazi kilichopo Wilaya ya Kibaha Mji Mkoani Pwani, wametakiwa kuiamini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuwa ni taasisi inayowapatia ufumbuzi wa changamoto zao zinazowakabili zinazohusiana na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Nyanda Shuli wakati akizungumza na Wananchi hao katika Mkutano wa hadhara leo Machi 13, 2025.

Mhe. Shuli amesema moja ya majukumu ambayo THBUB imepewa Kikatiba ni kupokea malalamiko na  kufanya Uchunguzi pale ambapo kuna uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

“Sisi THBUB tunatafuta ufumbuzi wa kero na  malalamiko ya wananchi yanayohusiana na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, ili THBUB ifanye uchunguzi lazima kuwe na watu ambao haki zao zimevunjwa na wameleta malalamiko kwetu” amesema Mhe. Shuli 

Aidha, Mhe. Shuli amesema Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura ya 391 inairuhusu THBUB kuanzisha uchunguzi wake yenyewe hata kama hayajaletwa mbele ya THBUB.

“Lakini hata malalamiko yasipoletwa mbele ya THBUB, Sheria inaturuhusu kushughulikia jambo ambalo tumelibaini kupitia vyanzo mbalimbali hata kama wananchi hawajalileta kwetu “ amesema Mhe. Shuli.

Katika mkutano huo wananchi wa Kijiji hicho wameishukuru THBUB kwa kufika Kijijini hapo na kuelezea changamoto wanazokutana nazo kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na viwanda vilivyopo katika kijiji hicho.