ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

Hali ya haki za binadamu inaendelea kuimarika

21 Jan, 2025
Hali ya haki za binadamu inaendelea kuimarika

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu  na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad, amesema kuwa hali ya haki za binadamu  nchini inaendelea  kuimarika kutokana na  uelewa wa watu juu ya haki za binadamu na utawala bora.

Akizungumza na Wanafunzi wa  Shule ya Sekondari ya Salmin Amour iliyopo katika  Manispaa ya Singida hivi karibuni alisema, hii ni kutokana na watu kuwa na uelewa wa kuibua masuala ya uvunjifu wa haki za binadamu.

"Watu wanaibua masuala mbalimbali yanatokea katika jamii lakini pia Serikali inachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa haki za watu zinalindwa" amesema Mhe. Mohamed 

Aidha, Mhe. Mohamed aliongeza kuwa THBUB inaendelea na jukumu la kutoa elimu kwa jamii na kufanya uchunguzi kwa lengo la kuzuia vitendo vya kikatili. 

 Katika hatua nyingine, Mhe. Mohamed ametoa wito  kwa Wazazi  kukomesha vitendo vya kikatili kwa Watoto ili kuendelea kulinda haki za mtoto.

Naye Mwalimu, Veronica Emmanuel ametoa shukrani kwa THBUB kwa kutembelea na kutoa elimu kwa wanafunzi na Walimu wa Shule hiyo kwani elimu hiyo itawasaidia Wanafunzi na Walimu kujua haki na wajibu wao ili waweze  kujisimamia nakufanya maamuzi sahihi hususan pale wanapokutana na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.