ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YATOA TAMKO KUHUSU KUPOTEA KWA WATU NCHINI

22 Aug, 2024
THBUB YATOA TAMKO KUHUSU KUPOTEA KWA WATU NCHINI

Kufuatia matukio ya kupotea kwa watu nchini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imesema inaendelea kufanya chunguzi maalum za matukio hayo kwa lengo la kubaini, pamoja na mambo mengine chanzo na wahusika ili kutoa mapendekezo stahiki.

Hayo amesema leo Agosti 22,2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu matukio hayo na kubainisha mikoa inayohusishwa na chunguzi hizo.

"Chunguzi hizo zinazoendelea kwa sasa zinahusisha mikoa ifuatayo Dar es Salaam, Singida, Mara, Simiyu,Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita, Kigoma, Tanga, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma na Rukwa, hatua hii ni mwendelezo wa chunguzi zinazohusu matukio ya kupotea kwa watu ambayo THBUB imekuwa ikiyafanyia kazi katika nyakati tofauti na taarifa zake kufikishwa katika vyombo vinavyohusika", amesema.

Aidha, Mhe.Mwaimu amesema kuwa  katika kufanikisha lengo la  taarifa  iliyotolewa  Julai 19,2024 iliyokuwa ikieleza  kazi ilizokuwa imetekeleza na THBUB  katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 hususan katika eneo la uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjifu wa haki za binandamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, THBUB ilikuwa imekwishafanya hatua mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa matukio hayo kwa maana ya sehemu yalikotokea na watu waliokuwa wanadaiwa kuhusika.

"Pia THBUB imeandaa mpango kazi wa namna ya kufuatilia matukio hayo kwa kuzingatia mamlaka yake na kuendelea na chunguzi kuhusu matukio hayo",amesema.

Aidha akizungumzia kuhusu vurugu zilizotolea siku ya jana Mkoani Simiyu zilizosababishwa na madai ya kupotea kwa watoto Mhe Mwaimu ameeleza kuwa THBUB itaendelea kufanya uchunguzi ili kuweza kulishughulikia suala hilo.

Tume ya haki za binadamu na utawala bora inatekeleza majukumu hayo chini ya ibara ya 130 (1)(b) na (c) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 6 (1)(b) cha sheria ya haki za binadamu na utawala bora sura ya 391.