THBUB YAKUTANA NA WADAU KUJADILI HAKI ZA WAVUVI WADOGO

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi katika mkutano maalum uliofanyika leo Julai 16, 2025, Jijini Dar es Salaam, kujadili haki za wavuvi wadogo wadogo katika upatikanaji na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wawakilishi kutoka Serikalini , asasi za kiraia, vyama vya wavuvi, wavuvi, wataalamu wa mazingira ya bahari, na mashirika ya kimataifa yanayoshughulika na maendeleo ya sekta ya uvuvi.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Uvuvi, Bi. Agness Meena aliyekuwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Prof. Mohamed Sheikh alisisitiza kuwa haki za wavuvi wadogo wadogo ni msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi nchini.
“Wavuvi wadogo ni mhimili mkubwa katika uchumi wa jamii za pwani na usalama wa chakula nchini. Ni wajibu wetu kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za bahari, wanalindwa dhidi ya unyanyasaji wa mifumo ya kisheria, na wanapewa elimu ya kutosha kuhusu matumizi endelevu ya bahari.”
Prof. Mohamed alisisitiza kuwa haki huenda sambamba na wajibu, hivyo tunapoelezea haki za wavuvi ni vyema pia tukaeleza wajibu wa wavuvi.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad alielezea namna changamoto za wavuvi wadogo zinaweza kutatuliwa ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii za wavuvi ili kuongeza uelewa wa haki za binadamu lakini pia kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ili kulinda haki za wavuvi wadogo wadogo.
Aidha, Mhe. Mohamed ameishauri Serikali kuwashirikisha wavuvi wadogo katika kupanga mikakati inayolenga kulinda rasilimali za bahari ili kutokiuka haki za binadamu .
“Ni muhimu Serikali kuwashirikisha wavuvi wadogo katika kupanga mikakati ya kulinda rasilimali za bahari ila kutokiuka haki za binadamu, hatua hii itachochea ukuaji wa uchumi.”
Mkutano huo umeandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Denmark ya Haki za Binadamu kwa lengo la kukuza uelewa wa pamoja juu ya jinsi haki za binadamu zinavyohusiana na upatikanaji na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo wadogo, kuunda muhtasari wa pamoja wa mijadala ya kitaifa na kubaini mbinu bora na suluhisho za changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo wadogo.