ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB yaendelea kukusanya maoni ya Mpango Kazi wa Kitaifa Haki za Binadamu na Biashara

25 Sep, 2024
THBUB  yaendelea kukusanya maoni ya Mpango Kazi wa Kitaifa Haki za Binadamu na Biashara

eo Septemba 24, 2024 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala (THBUB) imekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Isaya Tendega, Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Kagera.

Ujumbe wa THBUB  uliongozwa na Kamishna Mhe. Amina Talib Ali akiambatana na Bw. Chrisantus Ndibauokao, Afisa Uchunguzi Mkuu,  Bw. Mohamed Bakary, Afisa Uchunguzi Mkuu, wengine ni Bw. Efrazi Mkama kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Bw. Petro Maluwi kutoka UNICEF.

Mhe. Amina Talib alieleza kuwa lengo la ziara ya THBUB katika Mkoa wa Kagera ni Kuwashirikisha Wadau katika Uandaaji  wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu hususani katika eneo la Haki za Watoto.

Mhe. Amina Talib aliongeza kuwa THBUB imepewa jukumu la kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa  wa Biashara na Haki za Binadamu, na mpaka hivi sasa THBUB imefanya shughuli mbalimbali za ushirikishaji wa wadau ikiwemo kufanya vikao vya mashauriano na majadiliano na wadau mbalimbali, mikutano ya hadhara na wananchi wanaoishi karibu na  maeneo ya uwekezaji katika mikoa mbalimbali hapa Tanzania. Maeneo hayo ni Viwandani, Kilimo, usafirishaji, Uvuvi, Utalii, Taasisi za Serikali  na Binafsi.
"Serikali imeikabidhi THBUB jukumu la kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu lakini jukumu hili haliwezi kutekelezwa na THBUB peke yake bali ni lazima ishirikishe wadau wengine ili kufanikisha utekelezaji wa jukumu hili" Amesema  Mhe. Amina.

Aidha, Mhe. Amina Talib  amesema kuwa THBUB  imeona pia pamoja na kufuatilia haki nyingne katika biashara tumeona pia Uandaaji wa Mpango kazi huu uangalie haki za watoto.

"Kumekuwa na matukio ya kutumikishwa kwa watoto  katika maeneo mbalimbali ya biashara ambayo imefanya watoto hao  kuvunjiwa haki zao za msingi kama vile haki ya kupata elimu, haki ya kulindwa n.k, "amesema Mhe. Amina 

Kwa Upande  wake,  Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kagera Bw. Tendega amesema kuwa Kagera ni mkoa ambao uchumi wake unategemea uzalishaji katika sekta ya kilimo, Uvuvi na biashara.

Bw. Tendega ametoa pongezi  kwa THBUB kwa  kuja katika mkoa huo na kuchukua maoni kuhusu Biashara na Haki za Binadamu hususani katika  kuangalia eneo la haki za watoto.

“Nawapongeza THBUB na ninaimani   kuwa maoni mtakayopata kutoka kwa wadau yatasaidia katika Uandaaji wa Mpango Kazi huo hasa kwa upande  watoto ambao haki zao zinavunjwa wakati wanaposhirikishwa katika shughuli za uzalishaji” amesema.Bw.Tendega

THBUB inaendelea na ziara yake Mkoani Kagera na inatarajia kutembele na kufanya mazungumzo na Wawakilishi  wa Wavuvi katika Mwalo wa Nyamukazi lililopo katika  Manispaa ya Bukoba na Igabilo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya  Bukoba. Aidha THBUB itakutana na kufanya mazungumzo na Asasi za Kiraia,Kiwanda cha Sukari cha Kagera,  Wakulima  wa Miwa na jamii inayozunguka mashamba ya miwa.