Ziara ya THBUB Gereza la Mpwampwa
Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na taasisi simamizi zinazoratibu Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa umekabidhi mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Blanketi, Sabuni, Dawa za Meno na Taulo za Kike kwa Wafungwa na Mahabusu walio zuiliwa katika Gereza la Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Taasisi simamizi zinazoratibu maadhimisho hayo ni taasisi za utawala bora, mapambano dhidi ya Rushwa, Haki za Binadamu na uwajibikaji ambazo ni Ofisi ya Rais - Ikulu, Ofisi ya Rais- Management ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya katiba na Sheria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Desemba 6, 2024 Kamishna wa THBUB Mhe. Dkt.Thomas Masanja amesema kuwa mahitaji hayo yametolewa kwa ajili ya kuwasaidia Wafungwa na Mahabusu iliwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa ambayo kilele chake kitakuwa Disemba 10, 2024.
Pia Mhe. Dkt. Masanja ameongeza kuwa lengo la kutembelea Gereza hilo ni kuwakumbusha Maafisa wa Gereza hilo kuzingatia haki za binadamu kwa mahabusu na wafungwa waliopo Gerezani humo na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu ili kutatua changamoto zao zinazowakabili.
"Kuwa mfungwa hakuondoi Utu wake ,,,, japo kuna baadhi ya haki atakosa lakini haki ya utu ni lazima izingatiwe kwa kila mfungwa na Mahabusu" amesema Mhe. Dkt. Masanja.
Aidha Dkt. Masanja Amepongeza Gereza hilo, Mahakama na Jeshi la Polisi Wilaya ya Mpwapwa kwa kuhakikisha wafungwa waliopo wanapata haki yao ikiwa ni pamoja na haki ya kupewa Nakala ya hukumu kwa wakati na kutoa dhamana kwa wakati kwani kunasaidia kupunguza msongamano kwa mahabusu.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo SP. Justine S. Kipeta ameshukuru Ujumbe huo kwa kutimiza wajibu wa kisheria wa kutembelea Gereza hilo na kusema kuwa mahitaji hayo yamekuja wakati muafaka kwani wamekuwa wakipata Changamoto ya mahitaji hayo kutokana na wingi wa wafungwa.
Ziara hiyo ilishirikisha taasisi za Haki Jinai na Ustawi wa Jamii ambazo ni Mahakama ya Tanzania, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi Tanzania, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza.