WAZAZI WATAKIWA KUWA KARIBU NA WATOTO WAO HASA WA KIKE

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Dkt. Thomas Masanja amewataka wananchi ambao pia ni wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao hususan watoto wa kike.
Dkt. Masanja ametoa wito huo leo Machi 24, 2025 Mkoani Njombe, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi ya Mabasi Makambako iliyopo katika Halmashauri ya Mji Makambako.
“Wazazi tujaribu kuwa karibu na watoto wetu, na ukaribu huo lazima utaunda imani ya watoto wetu kwetu sisi wazazi ili mtoto anapofanyiwa vitendo vya ukatili aweze kuja kwetu wazazi na kutuambia “ amesema Dkt. Masanja
Aidha, Dkt.Masanja amewataka wananchi kuwa makini na watu wanaowakaribisha majumbani kwao maana asilimia kubwa ya vitendo vya unyanyasaji nakikatili hufanywa na ndugu wa karibu.
Aliendelea kusisitiza kwamba ikitokea ndugu wa karibu kafanya vitendo hivyo tusikae kimya na kuyamaliza kifamilia, inapaswa kutoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Katika mkutano huo wananchi walipata nafasi ya kutoa maoni yao ambapo waliiomba THBUB kuongeza ukaribu kwa wananchi na kuiomba THBUB kuwa inawatembelea mara kwa mara ili kutengeneza uelewa wa maswala ya haki za binadamu na utawala bora.