VIONGOZI THBUB WASHIRIKI MAFUNZO YA HAKI ZA BINADAMU NCHINI INDIA

Kamishna wa Tume za Haki za Binadamu, Mhe. Nyanda Shuli akiambatana na Katibu Msaidizi wa Tume Bw. Juma Karibona na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mawasiliano , Tafiti na Nyaraka, Bi. Monica Mnanka ni miongoni mwa Viongozi kutoka Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu kutoka nchi 11 ambao wamepata mafunzo kuhusu haki za binadamu nchini India hivi karibuni.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuzijengea uwezo taasisi hizo katika kulinda na kuhifadhi haki za binadamu yalifanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma kwa ufadhili wa Tume ya Haki za Binadamu ya India ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya nje ya nchi hiyo kuanzia Machi 03 hadi 08, 2025
Katika kipindi hicho, viongozi hao walijifunza kuhusu masuala ya haki za binadamu yanayoendelea kujitokeza katika zama hizi zilizotawaliwa na maendeleo makubwa ya teknolojia, ulinzi wa haki za makundi maalum katika jamii, nafasi ya mtandao na haki za binadamu, upatikanaji wa huduma za afya, demokrasia na chaguzi huru vinavyohusiana na haki za binadamu.
Mambo mengine waliojifunza ni pamoja na jinsi ya kushughulikia malalamiko, uvunjifu wa haki za binadamu, uchunguzi, ushirikiano wa Tume na Asasi za kiraia katika kutetea haki za binadamu na uchambuzi wa taarifa za haki za binadamu.
Katika mafunzo hayo, nchi wenyeji India waliweza kueleza namna ambavyo imeweza kuhifadhi haki za binadamu nchini humo, kujengea uwezo nchi nyingine katika kuhifadhi haki hizo na namna inavyoshirikiana na asasi na jumuia mbalimbali katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuhifadhiwa.
Utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu kutoka nchi mbalimbali ni moja ya mafanikio ambayo nchi ya India inajivunia kwa kutumia uzoefu wake katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya mipaka ya nchi yao pamoja na kuwezesha washiriki kubadilishana uzoefu.