ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YAENDELEA NA KAZI  MKOANI DODOMA

26 Mar, 2025
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YAENDELEA NA KAZI  MKOANI DODOMA

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelenga kuongeza uelewa kwa Watendaji wa Kata katika Mkoa wa Dodoma juu ya Malalamiko yanayoripotiwa katika Ofisi zake.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Nyanda Shuli Machi 25, 2025 alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bwa. Kaspar Mmuya kwa lengo la kumfahamisha Shughuli zinazoendelea kufanywa na THBUB Mkoani humo.

Mhe. Shuli ameeleza kuwa THBUB inatarajia kuanza kutoa elimu ya Haki za Binadamu na misingi ya utawala bora kwa wananchi, Watendaji na Wanafunzi wa shule za sekondari ili kuweza kuwapa fursa ya kutambua haki na wajibu wao katika jamii.

Katika Ziara hiyo Mhe. Shuli amesema kuwa THBUB itakuwa na jukumu la kuwajengea uwezo wananchi na watendaji juu ya haki za binadamu, kukagua Gereza la King’ang’a na kufungua vilabu vya Haki za Binadamu kwa baadhi ya Shule za Sekondari zitakazofikiwa.

“THBUB inakwenda kwa wananchi kutoa Elimu na kuwaeleza kuwa wanapokuwa na changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu basi watambue kuwa Tume ipo tayari kuwasaidia na wajue njia sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao” amesema Mhe. Shuli.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bwa. Kaspar Mmuya ameipongeza THBUB na kusema kuwa zoezi hilo litakwenda kuamsha ari ya Watendaji katika Kutenda kazi kwa kuzingatia haki za binadamu.