ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YATOA WITO KWA ASKARI KUSIMAMIA HAKI

16 Sep, 2025
THBUB YATOA WITO KWA ASKARI KUSIMAMIA HAKI

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa wito kwa Jeshi la Polisi kusimamia uhuru, haki na amani ili wananchi waweze kutimiza haki yao ya kikatiba katika kuchagua viongozi wao.

Wito huo umetolewa leo Septemba 16,2025 hapa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akifungua mafunzo kwa maafisa wa Jeshi la Polisi kuhusu uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika mchakato wa uchaguzi mkuu 2025.

"Katika kipindi hiki cha uchaguzi, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima, baadala yake kuhakikisha usalama wa watu na mali zao katika kipindi chote cha uchaguzi", "amesema. 

Amesema mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi ambapo wananchi watapata fursa ya kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi za uongozi hivyo ili uwe huru na wa haki kabla, wakati na baada ya hatua hiyo haki za binadamu zinapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.

"Kwa kuzingatia ibara ya 130(1)(a) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 6(1)(a) na (d) cha sheria ya THBUB, sura ya 391, Tume hiyo inalo jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora, "amesema. 

Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia maafisa hao kutimiza wajibu wao na kuhakikisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora inazingatiwa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi. 

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma Mjini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Grace Salia amesema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia haki za binadamu hususani kipindi hiki cha Kampeni na kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025. 

"Tutazingatia sheria, taratibu na kanuni pamoja na kuangalia haki za binadamu ukizingatia kuwa nchi yetu imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusiana na haki za binadamu, "amesema. 

Naye, Afisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi William Mwamafupa amesema wataendelea kuzingatia haki za binadamu katika kutekelezaji wa majukumu yao. 

Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa maafisa hao wa Jeshi la Polisi kama maafisa wa utekelezaji wa sheria kuhusu umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora wakati wa kutekeleza majukumu yao hasa katika uchaguzi ujao.