THBUB YAHIMIZA USHIRIKIANO NA ASASI ZA KIRAIA ZINAZOTETEA HAKI ZA BINADAMU

KAMISHNA, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ofisi ya Zanzibar, Mhe. Khatib M. Mwinyichande, amesifu ushirikiano uliopo baina ya tume na Jumuiya zisizo za Serikali zinazotetea haki za binaadamu
Amesema, ushirikiano wao utaongeza nguvu ya pamoja katika kueneza elimu kwa umma ili kuifika jamii iliyokusudiwa kwa wakati.
Aidha, ameeleza kuwepo kwa nguvu ya pamoja juu ya mapambano ya utetezi wa haki za binaadamu zinahitajika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na taasisi hizo.
Mhe. Mwinyichande aliyasema hayo kwenye mkutano wa pamoja wa ushirikiano baina ya taasisi za haki jinai na watetezi wa haki za binaadamu wakiwemo wenyeji Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora, (THBUB), Jumuiya ya Mawakili Zanzibar - (ZLS), Jumuiya Wanasheria wa Afrika, Jumuiya ya Mawakili kutoka Afika Mashariki, (EALS) na Chama cha Wanasheria Wanawake, Zanzibar (ZAFELA) kikao kilichofanyika ofisi za (THBUB) Mbweni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza, ushirikiano wao utachochea nguvu ya pamoja kwenye mapambano dhidi ya uvunjifu wa haki za watu.
Aidha, aliongeza kuwa ukaribu wa taasisi hizo katika kubadilishana uzoefu na kutambua zaidi michango yao hasa kwenye utetezi na upatikanaji wa haki za binaadamu na kutoa elimu kwa wadau wengine wa haki za binaadamu ili kujua mipaka na wajibu wao wa kutenda haki na kuheshimu misingi ya utawala bora.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Naibu Katibu Mtendaji THBUB, Juma Msafiri Karibona amezishukuru taasisi hizo kwa ujio wao kwenye ofisi za THBUB sambamba na kusisitiza ushirikiano wao hasa kwenye utetezi wa haki za binaadamu.
Naye, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa - amepongeza jitihada za pamoja zinazopambania haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kutoa rai ya kuelekezwa zaidi nguvu ya pamoja kwenye uchunguzi na kuchukuliwa hatua za haraka endapo kutabainika uvunjifu wa haki za binaadamu.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi na Afisa Mchunguzi Mkuu (THBUB) Zanzibar, Saada Ahmeid Masoud pia amehimiza zaidi ushirikiano kwenye utetezi wa haki za binaadamu.
Taasisi nyengine zilizoshiriki kwenye mkutano huo wa pamoja wa ushirikiano katika utetezi wa haki za binaadamu ni East Afican Law Society (EALS), Pan African Lawyers Union (PALU), Chama cha Wanasheria Wanawake (ZAFELA) na Tanganyika Law Society (TLS).