ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB yatembelea hospitali ya Mirembe na kutoa msaada

22 Mar, 2024
THBUB yatembelea hospitali ya Mirembe na kutoa msaada

 

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ujumbe wa watumishi wanawake kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) leo Machi 15, 2024 umetembelea Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe jijini Dodoma na kutoa msaada.

Akiongea wakati wa kukabidhi bidhaa mbalimbali Kiongozi wa ujumbe huo, Kamishna wa Tume, Mhe. Amina Talib Ali alisema kuwa lengo la ziara yao ni kuwafariji nakuwashika mkono wagonjwa wenye uhitaji maalum hosptalini hapo.

Aidha, Mhe. Amina, ambaye pia ni Msimamizi wa masuala ya makundi maalum katika THBUB alitoa pongezi kwa madaktari, wauguzi na watumishi wengine kwa kuwathamini na kujitoa kwao kuwahudumia wagonjwa waliopo hospitali hapo.

Mhe. Kamishna aliukabidhiuongozi wa hospitali ya Mirembe bidhaa zenye thamani ya jumla ya Shs. 610,000/=, zikijumuisha: sabuni za kufulia na kuogea, pampasi za watoto, mafuta ya kupaka, na maziwa. Bidhaa nyingine ni miswaki, dawa za meno, nguo za ndani, pamoja na unga wa lishe.

Akipokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Godwin Mwisombe aliishukuru THBUB kwa kuwakumbuka wahitaji waliopo hospitalini hapo. “Msaada huu ni wa muhimu sana na utasaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizopo,” alisema.

Dkt. Mwisombe alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa umma kujiepusha na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ugonjwa wa akili na kuunga mkono jitihada za kuelimisha umma juu ya changamoto ya afya ya akili, ambayo inawakumba watu wengi kila uchao.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo watu wengi wana changamoto ya afya ya akili, na wachache ndiyo wenye ugonjwa wa akili, hivyo elimu inahitajika ili kulikinga kundi hilo kubwa lisipatwe na ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii hospitalini hapo, Bi. Irene Kitula alitoa wito kwa taasisi nyingine na watu binafsi kuiga mfano wa THBUB ili kuiwezesha hospitali hiyo kuwahudumia kikamilifu wagonjwa, ambapo baadhi yao wametekelezwa na familia zao.

Mwaka huu kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake yalifanyika kimkoa Machi 8 Viwanja vya Shule ya Chinangali wilayani Chamwino ambapo THBUB ilishiriki pia.