ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB yaipongeza Serikali kwa kuendeleza haki za Wanawake

10 Mar, 2024
THBUB yaipongeza Serikali kwa kuendeleza haki za Wanawake

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kutekeleza haki na utu wa mwanamke nchini.

Imezitaja hatua hiyo kuwa ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na ajira, kuhakikisha usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, na kupambana na ukatili wa kijinsia na mila kandamizi.

Hayo yameelezwa kwenye taarifa iliyotolewa jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mohamed Khamis Hamadleo Machi 8, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali,taarifa hiyo imeeleza kuwa bado zipo changamoto kadhaa zinazowakabili Wanawake hapa nchini.

Imezitaja changamoto hizo kuwa ni uchache wa Wanawake katika nafasi za ajira na uongozi, uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, uwepo wa mila na desturi kandamizi, Wanawake wenyewe kushindwa kuthubutu na kujiamini katika kuwania nafasi za uongozi, umasikini, na ushirikishwaji duni katika kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia.

Kutokana na changamoto hizo, Tume  inapendekeza kuwa Serikali itekeleze mikataba yote ambayo nchi imeridhia, taarifa hiyo imeeleza.

Pia, inapendekeza kuwa Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar, kuendelea kuongeza ushiriki wa Wanawake katika uwekezaji na biashara ili kuchochea maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Vilevile, Tume imetoa wito kwa Asasi za kiraia, mashirika ya Kidini na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mila kandamizi zinazochangia Wanawake kubaki nyuma kimaendeleo.

Mkoani Dodoma maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali Wilayani Chamwino na yameongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaulum, Mhe. Dorothy Gwajima akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa kama Mgeni Rasmi.