ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

Jaji Mwaimu alitaka Baraza la wafanyakazi THBUB kutoa elimu kuhusu wajibu

16 Feb, 2024
Jaji Mwaimu alitaka Baraza la wafanyakazi THBUB kutoa elimu kuhusu wajibu

 

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.) amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume kuwaelimisha watumishi wenzao na wananchi kutimiza wajibu wao.

Pia, aliishauri Menejimenti ya Tume kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotekeleza wajibu wao, kutoa kipaumbele katika kushughulikia changamoto za watumishi, na kuandaa mpango endelevu wa mafunzo.

Mhe. Mwaimu ameyasema hayo leo Februari 15, 2024 wakati akifungua mkutano wa 22 wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB uliofanyika kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma.

Kwa vyovyote vile hakuna haki bila wajibu, kwa hiyo tuna kazi kubwa kuhakikisha kuwa ... wanaohitaji haki tunawasaidia na kuwaelimisha kuhusu wajibu wao wa kufuata sheria na taratibu za kupata haki,” Mhe. Mwenyekiti aliwaambia wajumbe wa Baraza, “huu wajibu ni kwa ... watumishi na ... wadau wetu.”

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mwaimu Menejimenti inapochukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wasiowajibika ipasavyo husaidia kuhakikisha majukumu ya taasisi husika yanatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Akizungumzia changamoto za watumishi, Mheshimiwa Mwenyekiti alibainisha kuwa changamoto hizo ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, madai ya likizo, kupandishwa vyeo, na maslahi bora.

Kuhusu mafunzo alisema: “Ofisi ya Katibu Mtendaji wa Tume  iendelee kuwahimiza watumishi kujiendeleza na kupata mafunzo ya muda mrefu au mfupi ili kuongeza ujuzi na maarifa katika maeneo yao ya kazi ... nawashauri kuandaa mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa watumishi ... kutegemeana na uwezo uliopo wa kifedha.”

Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu alitumia fursa hiyo pia kuhimiza kuhusu uzingatiajiwa sheria, taratibu, kanuni za maadili ya utumishi wa umma,kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, na kutoa huduma bila upendeleo wowote.

Awali Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Patience Ntwina alieleza kuwa pamoja na masuala mengine mkutano huo utapokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa vipindi vya 2022/2023 na 2023/2024; taarifa ya makadirio ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha (2024/2025); na pia watajadili hoja za watumishi.

Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha takriban wajumbe 55 kutoka makao makuu ya Ofisi za Tume Dodoma, Ofisi ya Tume Zanzibar na Ofisi za Tume za matawi ya Dar es Salaam, Lindi, Pemba na Mwanza.