08
Wed, Apr
6 New Articles

Mwaimu atembelea mabanda ya wadau

Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Jaji (mstaafu) Matthew Mwaimu akipokea machapisho kutoka kwa Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alipotembelea banda la kituo hicho katika maonesho ya Wiki ya Sheria viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma Februari 1, 2020. Kulia ni Afisa wa Tume, Bwana Joshua Mwambande aliyekuwa ameambatana na Mwenyekiti huyo wa Tume.

News
Typography

HAKIKA uongozi wa Awamu ya Nne wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora umedhamiria kukuza ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi. Hili limethibitishwa leo (Februari 1, 2020) kwa hatua ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, kutenga muda wa kutembelea mabanda ya baadhi ya wadau wake wanaoshiriki maonesho ya Wiki ya Sheria  yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.

 

Mwenyekiti huyo, Mhe. Jaji (mstaafu) Matthew Mwaimu alifanya ziara hiyo mara baada ya hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria kwa umma kumalizika na viongozi na wageni waalikwa kutawanyika.

“Habari zenu vijana! Mimi ni Jaji mstaafu Matthew Mwaimu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nimepita kuwasalimu na kujifunza kuhusu huduma zenu,” alisema kila alipowasili kwenye mojawapo ya mabanda matatu (3) aliyofanikiwa kuyatembelea.

Mabanda hayo matatu (3) ambayo Mhe. Mwaimu amefanikiwa kuyatembelea ni ya taasisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Kituo cha Amani, Msaada wa Kisheria na Haki (Tanzania Peace, Legal Aid & Justice Centre – PLAJC).

Maafisa waliokuwa wakitoa huduma kwenye mabanda hayo, hata wale ambao walikuwa hawamfahamu vizuri hapo kabla walimpokea kwa bashasha na kumpa maelezo ya kina kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao na kumfungashia machapisho mbalimbali.

Mwenyeketi huyo wa Tume aliwapongeza maafisa hao kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao na kwa kuwasaidia kuzipata. Aidha, aliahidi kufanya ziara rasmi ya kuzitembelea taasisi hizo katika ofisi zao.

Leo ni takriban siku 90 tangu uongozi wa Awamu ya Nne wa Tume uingie madarakani; na hadi sasa uongozi huo umekwisha tembelea taasisi wadau wa ndani zaidi ya 15, na umetembelewa na zaidi ya taasisi tatu (3) za nje. Ziara ya mwisho ni ile iliyofanywa kwa mara ya kwanza, mapema wiki hii na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu Afrika (NANHRI), Bwana Gilbert Sebihogo.

Ushirikiano na wadau katika kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini ni mojawapo ya mikakati ya Tume inayolenga kuongeza ufanisi na tija katika utoaji huduma kwa wananchi. Tume inaamini kuwa kwa kushirikiana na wadau itaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani ya muda mfupi.

Kwa msingi huo mwaka 2018 Tume iliandaa Mkakati wa Mashirikiano na Wadau (Stakeholders Engagement Strategy) na kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano na Asasi za Kiraia 21 katika utoaji wa elimu ya haki za binadamu na utawala bora kwa umma, usambazaji wa taarifa na ufuatiliaji wa uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.