05
Sun, Jul
7 New Articles

THBUB yahimizwa kushirikiana na serikali kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi

Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI, Gilbert Sebihogo (Kushoto) akikaribishwa na mwenyeji wake Mwenyekiti wa THBUB Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu (Kulia) katika ofisi za THBUB jijini Dodoma.

News
Typography

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa taasisi ya Haki za Binadamu Afrika (NANHRI), Gilbert Sebihogo ameishauri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kushirikiana na serikali katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi, huku akiwaasa  kujiepusha na vitendo vya kukosoa kila jambo linalofanywa na Serikali. 

Sebihogo alitoa kauli hiyo Januari 30, 2020 katika ofisi za THBUB zilizopo Dodoma alipozitembelea  kwa lengo la kutambuana na Makamishna  wa tume  na kuimarisha uhusiano wao wa muda mrefu . 

Alimueleza Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu kuwa tume itafute namna nzuri ya kuishauri  serikali na kujenga ushawishi utakaofanya serikali iendelee kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

“Tume mnapaswa kuendelea kuishawishi serikali kufanya nao kazi kama washirika, mfanye kazi bila misuguano wala kudharau mambo mazuri yanayofanywa na serikali, kwa kufanya hivyo kutaifanya serikali kushirikiana na nyinyi”, Sebihogo alisisitiza

“Msiwe wakosoaji wa  kila jambo kama baadhi ya watu au taasisi nyingine zinavyofanya, kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa na serikali, hamna budi kutambua juhudi hizo na pale mnapoona kuna jambo ambalo alijafanywa vizuri na serikali toeni maoni yenu kwa busara, alieleza Sebihogo

Aliongeza kuwa sio jambo rahisi kwa taasisi nyingi za haki za binadamu kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali bila misuguano, lakini inawezekana kwa kutumia njia nzuri za kuishawishi serikali kujua kuwa taasisi ya haki za binadamu ipo kwa ajili ya kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake na sio vinginevyo.

“Tume ni muhimu kutambulika na serikali na wananchi, ifanye kazi kwa kuwafikia wananchi wa kawaida hadi ngazi za chini, ikifanya hivyo watu watashawishika kuja kwenu kupata huduma na hata zile taasisi zenye majukumu kama yenu zitashawishika kuja  kupata maoni na ushauri”aliongeza

Sebihogo aliendelea kusisitiza kuwa THBUB ikipoteza uhalali wake kwa wananchi,  wengine watapaza sauti zao, na wataisemea  THBUB, kitu ambacho sio sawa, lakini tume ikifanya kazi zake ipasavyo taasisi zote zenye majukumu sawa na tume zitawaunga mkono. 

Akiongezea hapo, aliieleza THBUB kuwa kupitia mamlaka iliyopewa inayo nafasi ya kushiriki kuisaidia serikali kutimiza  malengo makubwa iliyojiwekea.

Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alimwambia Sebihogo kuwa tangu walipoteuliwa kuwa Makamishna wa THBUB wamefanya mbalimbali za kujaribu kukutana na viongozi mbalimbali  kwa lengo la kutafuta ushirikiano na mpaka sasa juhudu hizo zinaenda vyema. 

“Tutaendelea kutafuta fursa za kukutana na kukaa pamoja na serikali ili kuwaelewesha waweze kutambua mamlaka na majukumu ya tume, tunajua kuwa kuna maeneo bado tunahitaji kuyaboresha ili kushirikiana bega kwa bega na serikali, wadau na jamii kwa ujumla” Jaji Mwaimu alisema

Makamu Mwenyekiti wa tume, Mohamed Hamad pia alisisitiza kuwa THBUB inaunga mkono jitihada za serikali katika kuwapatia haki za msingi wananchi.

“Sisi tume tunaunga mkono jitihada za serikali, na ni wazi kuwa  tume ni taasisi ya umma iliyopewa mamlaka ya kuisaidia serikali kuhamasisha na kulinda haki za binadamu nchini”, Hamad alifafanua

Aidha, Hamad aliiomba NANHRI kama mtandao wa haki za binadamu kuhamasisha wanachama wake kudumisha mila na desturi za kiafrika na kuachana na baadhi ya haki zinazohamasishwa na nchi za magharibi na ulaya ambazo zipo kinyume na tamaduni za waafrika. 

Mtandao wa taasisi ya Haki za Binadamu Afrika (NANHRI) ni taasisi muamvuli ya kikanda iliyoanza kazi mwaka 2007 yenye makazi yake nchini Kenya na ina wanachama 44 kutoka nchi za afrika ikiwemo Tanzania. 

Jukumu la Mtandao huu ni kusaidia na kuimarisha taasisi za haki za binadamu za Afrika kwa kuziwezesha na kuhakikisha zinashirikiana zenyewe na taasisi nyingine za kimataifa.

Mwis

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.