08
Wed, Apr
6 New Articles

Wananchi changamkieni fursa, muelewe haki zenu! – Ndugai

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (katikati) pamoja na mwenyeji wake, Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma (watatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Sheria Februari 1, 2020 viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Wa tatu kutoka kushoto (waliosimama) ni Mhe. Jaji (Mstaafu) Matthew Mwaimu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

News
Typography

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya maadhimisho ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria yaliyoanza leo kote nchini kujua haki na wajibu wao.

Mhe. Ndugai ametoa wito huo leo (Februari 1, 2020) katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma akizindua maadhimisho hayo ambayo yanahusisha maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau wa sheria nchini, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za kisheria.

“Huu ni wakati wa wananchi muweze kuelewa haki...pia... wajibu wenu,” alisema Mheshimiwa Spika katika hotuba yake wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa maadhimisho hayo iliyotanguliwa na matembezi ya takriban kilometa tano (5).

Aidha, Mhe. Ndugai alibainisha kuwa wananchi wakiwa na uelewa wa kutosha wa haki zao na taratibu za kimahakama hawataweza kudanganywa kirahisi, na kamwe hawataziogopa mahakama.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma amewataka wenye dhamana ya kutekeleza sheria nchini kuitumia wiki hii ya maadhimisho ya elimu ya sheria kuchunguza sheria mbalimbali za nchi na kuona iwapo kuna vizuizi ili vizuizi hivyo viweze kuondolewa mapema badala ya kusubiri hadi wananchi wapeleke madai mahakamani.

Mhe. Jaji Mkuu pia amekemea vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kutekeleza sheria kwa mtindo wa kufanya operesheni, mfano operesheni ya nyumba hadi nyumba. Watumishi wa aina hii hawafai kuwa katika nafasi walizopo, kwa mujibu wa Mhe. Jaji Mkuu.

“Sheria haitekelezwi kwa operesheni...wakati hujamweleza huyo mwananchi sheria inasema nini ili awe katika mizania sawa ya sheria...;” Mhe. Prof. Juma amesema.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria nchini ambayo kilele chake ni Februari 6, 2020 yamebeba kauli mbiu isemayo: “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na wadau kuweka mazingara wezeshi ya uwekezaji.”

Zaidi ya taasisi 30, ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora zinashiriki katika maadhimisho hayo ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria yanayoendelea hadi Februari 5, 2020 viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.