05
Sun, Jul
7 New Articles

Jaji Mwaimu akutana na Waziri Mkuchika

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Kapt. (Mst), George Huruma Mkuchika (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Waziri huyo Mtumba, Dodoma Januari 24, 2020. Kushoto anayewatazama ni Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mohamed Hamad, na wengine katika picha ni watendaji wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

News
Typography

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Kapt. (Mst), George Huruma Mkuchika Januari 24, 2020.

Jaji Mwaimu alimtembelea  Waziri Mkuchika ofisi kwake  Mtumba, Dodoma kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kufanya kazi na kuimarisha ushirikiano baina ya ofisi hizo mbili.

Akizungumza katika kikao hicho kifupi, Jaji mwaimu alimueleza Mkuchika kuwa waliona ni vyema  kukutana nae kwa kuwa yeye ndio waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa misingi ya utawala bora nchini kazi ambayo tume nao wanaifanya.

“Mheshimiwa Waziri  tumekutembelea ili utufahamu, pia kujenga mahusiano ya kazi kwa kuwa sisi sote kimsingi tunashughulika na  masuala ya usimamizi wa misingi ya utawala bora nchini”, alisema Jaji Mwaimu

“Tume tumekuwa tukipokea  malalamiko mbalimbali yanayohusiana na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na tumekuwa tukiyashughulikia vyema ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao”, alieleza  Mwenyekiti huyo

“Mheshimiwa,  tume katika utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti, lakini tunaendelea kujitahidi kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu inavyopaswa ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi tunao wahudumia” Jaji Mwaimu aliongeza 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mohamed Hamad alimueleza Waziri Mkuchika kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao tume imekuwa ikikumbana na changamoto ya baadhi ya taasisi za serikali kutokujibu barua za tume kwa wakati, na  hivyo alimuomba waziri huyo kusaidie kuzitaka taasisi hizo kujibu barua kwa mujibu wa sheria na taratibu zinavyotaka.

“Mheshimiwa waziri kuna baadhi ya taasisi zinatukwamisha kwa kutokujibu  barua zetu pindi tunapowaandikia kutaka maelezo kuhusiana na malalamiko yanayotufikia, tunakuomba  utusaidie kuwakumbusha kutimiza wajibu wao”alisema Hamad

Akiongea katika kikao hicho, Waziri Mkuchika aliwahakikishia tume kuwa ofisi yake itashirikiana kwa ukaribu na tume kwa kuwa wote wanashughulika na masuala ya utawala bora, na alisema kuwa watashirikiana  sio kama hisani bali ni wajibu wao kufanya hivyo na kuongeza kuwa Mheshimiwa Rais amekuwa akiwasisitiza sana kushirikiana ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Mkuchika alimueleza Mwenyekiti wa tume kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi yanayohusiana na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kuongezeko kwa malalamiko haya  kunatokana na kazi inayofanywa na taasisi hizo katika kuelimisha wananchi kujua haki zao na kuzidai, aidha utandawazi na uwazi serikalini umekuwa chachu kubwa kwa ongezeko hilo.

Kikao hicho kimejuisha Makamishna wa tume na viongozi wake pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.