04
Tue, Aug
3 New Articles

Makamu Mwenyekiti THBUB awataka vijana kushiriki katika utekelezaji wa SDGs

Mhe. Mohamed Khamis Hamad Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), akifafanua jambo kuhusu kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu lililofanyika Ofisi za Tume Dar es salaam leo tarehe 11/12/2019.

News
Typography

 MAKAMU Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mohamed Khamis Hamad amewataka vijana nchini kuyaelewa malengo endelevu ya maendeleo (SDGs) ili waweze kushiriki kikamilifu kuyatekeleza

Mhe. Hamad alitoa wito huo Desemba 12, 2019 jijini Dar es Salaam katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu lililokusudia pamoja na mambo mengine kuongeza uelewa wa vijana, hususan wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuhusu lengo endelevu Na. 16 la SDG na kubadilishana mawazo.

Kongamano hilo lililowajumuisha takriban washiriki 60 kutoka vyuo sita vya elimu ya juu vilivyoko jijini Dar es Salaam limefanyika kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya haki za binadamu kimataifa, ambayo kilele chake kilikuwa Desemba 10, 2019.

Lengo endelevu Na. 16 linahusu kukuza jamii zenye amani na umoja kwa maendeleo endelevu na kutoa fursa ya upatikanaji wa haki kwa wote kwa kujenga taasisi bora, zinazowajibika na zilizo jumuishi katika ngazi zote.

Mhe. Makamu Mwenyekiti wa Tume alibainisha kuwa ongezeko la uelewa wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuhusu lengo endelevu Na. 16 itakuwa chachu kwa vijana na wananchi kwa ujumla katika kuleta maendeleo endelevu katika nyanja mbalimbali za kijamii hapa nchini.

Pia alibainisha kuwa ongezeko hilo la uelewa litaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya  aina mbalimbali za dhuluma na ukatili dhidi ya wanawake na mtoto wa kike, ndoa na mimba za utotoni na unyanyasanji wa aina mbalimbali vyuoni na katika jamii kwa jumla.

Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu kanda ya Afrika Mashariki.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.