04
Tue, Aug
3 New Articles

THBUB, AZAKI kuandaa taarifa ya pamoja

Kaimu Katibu Mtendaji, Hajjat Fatuma Muya (katikati) akiongea katika warsha ya kupeana mrejesho wa kazi za robo mwaka (Julai-Septemba) iliyofanyika kwa siku tatu (3), kuanzia Oktoba 21—23, 2019 Mkoani Morogoro. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka kutoka Tume, Alexander Hassan, na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Mipango kutoka Tume, Laurent Burilo.

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia (AZAKI) washirika wamekutana  Mkoani Morogoro kuandaa taarifa ya pamoja ya robo mwaka ya kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2019 ya hali ya haki za binadamu nchini.

 Akifungua warsha hiyo ya siku tatu, iliyoanza Oktoba 21—23, 2019, Kaimu Katibu Mtendaji,Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya alisema kuwa  warsha hiyo imelenga katika  kupeana mrejesho wa kazi walizofanya tangu ushirikiano wao uanze, mrejesho huo ndio utakaotumika kuandaa taarifa ya pamoja  ya robo mwaka ambayo baada ya kukamilika kwake itasambazwa kwa wadau mbalimbali. 

 Taarifa hiyo itakayoandikwa itakuwa ni ya kwanza na ya kipekee tangu kuanzishwa kwa ushirikiano huu, kwani kupitia taarifa hiyo jamii itaweza kuona na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi zetu katika kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini” alisema Muya

Muya aliendelea kusema kuwa Tume inaamini katika kufanya kazi kwa kushirikiana kwani wanaamini ndio njia pekee ya kuweza kufikia matokeo makubwa yanayoweza kuonekana kwa haraka.

“Natambua kazi nzuri mnazozifanya katika kusaidia jamii kwenye maeneo yanu ya kazi na mmekuwa mkitoa taarifa za utekelezaji, lakini uamuzi huu wa kuwa na taarifa ya pamoja utafanya umoja wetu kutambulika zaidi na jamii itaweza kuona ni kwa kiasi gani wameweza kusaidiwa; hususani katika maeneo ya utoaji wa msaada wa kisheria na elimu kwa umma” aliongeza Muya

 Wakati huohuo, Muya aliwakumbusha AZAKI washirika kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali na walizojiwekea kama washirika katika utekelezaji wa majukumu yao, kwani ni kwa kufanya hivyo tu ndio wataweza kuudumisha ushirikiano huo.

“Mkutano huu ni mwafaka kwetu kwa kuwa pia tunapata fursa ya kujikumbusha wajibu wetu katika kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu” alisisitiza

Aidha, Muya aliwaomba AZAKI washirika wakati wanatekeleza majukumu yao waendelee kuitangaza Tume, kwani Tume peke yake haiwezi kufanya kila kitu na ndio maana iliona ni muhimu kuanzisha ushirikiano huo. 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilitiliana saini ya ushirikiano na AZAKI 20 Julai, 2018, na warsha hii iliyofadhiliwa na Shirika la Maendelea la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni miongoni mwa utekelezaji wa majukumu yao kulingana na makubaliano ya ushirikiano huo. 

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.