03
Mon, Aug
3 New Articles

AZAKI wahimizwa kuitumia THBUB

Wakili Clarence Kipobota akisisitiza jambo katika kikao kazi cha siku tatu cha kupeana mrejesho wa kazi walizofanya kati ya Tume na AZAKI na kuandaa taarifa ya pamoja ya robo mwaka ya hali ya haki za binadamu nchini kilichofanyika Mkoani Morogoro, Oktoba 21—23, 2019.

News
Typography

Asasi za Kiraia (AZAKI) zimeshauriwa kuitumia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kufikisha taarifa kwa jamii kwani ndio taasisi pekee ya kitaifa iliyokasimiwa mamlaka ya kulinda, kuhifadhi, kutetea na kuhamasisha haki za binadamu nchini.

 

Rai hiyo ilitolewa na Wakili Clarence Kipobota katika kikao kazi cha siku tatu cha kupeana mrejesho wa kazi walizofanya kati ya Tume na AZAKI na kuandaa taarifa ya pamoja ya robo mwaka ya hali ya haki za binadamu nchini kilichofanyika Mkoani Morogoro, Oktoba 21—23, 2019.

Akiongea katika kikao kazi hicho, Kipobota, ambaye alikuwa mwezeshaji aliwahimiza AZAKI kuitumia tume kama sehemu yao ya kufikishia taarifa.

“Tume haina mshindani, na AZAKI hazishindani na tume, kwa kuwa ndio taasisi iliyopewa mamlaka ya kusimamia masuala ya haki za binadamu na utawala bora nchini, hivyo tuitumie kufikishia taarifa zetu kwa jamii” alisema Kipobota

Aliongeza kuwa AZAKI zinafanya kazi nzuri sana ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii nchini na kuwasisitiza kuendelea kufanya hivyo na kutumia ushirikiano wao na tume kubadilishana taarifa zitakazoendelea kusaidia jamii.

“Mnafanya kazi nzuri sana, lakini kufanya kazi kwa kushirikiana na tume kutawaongezea hadhi, kutambulika na kuaminika zaidi” aliongeza Kipobota

Kama unataarifa usizifiche, zitoe na uzifikishe kwa tume, hii ni fursa nzuri kwenu AZAKI kushirikiana na tume.Itumieni. alisisitiza Kipobota.

Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na tume kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kilimalizika Oktoba 23, 2019 kwa kupeana mrejesho wa kazi zilizofanywa na taasisi hizo na kufanikiwa kuandaa taarifa ambayo itakapokamilika itasambazwa kwa wadau mbalimbali.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.