05
Fri, Jun
5 New Articles

Mkuchika aonya watumishi wasio waadilifu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika akiongea kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika kitaifa jijini Dodoma, Desemba 11, 2019.

News
Typography

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ametoa onyo kwa watumishi wasio waadilifu na kusema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao pindi watakapobainika.

Mkuchika alitoa onyo hilo Desemba 11, 2019 kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika kitaifa jijini Dodoma.

 

Alisema katika kongamano hilo kuwa ni kosa kisheria kwa mtumishi wa umma kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma na kuwataka kujiweka mbali na vitendo hivyo kwani watakaobainika serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.

“Katika kuhakikisha serikali ya awamu ya tano inajenga na kuimarisha uadilifu wa watumishi, serikali ilifanya uhakiki wa watumishi na kwa kipindi cha miaka minne imeweza kuwaondoa kazini watumishi hewa na wenye vyeti bandia elfu nne”alisema Mkuchika

Mkuchika aliendelea kusema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha maadili yanazingatiwa na watumishi wote.

Alisema serikali imetunga sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha maadili yanazingatiwa kwa lengo la  kujenga utawala bora.

“Maadili ni nguzo muhimu katika utumishi wa umma, ndio maana serikali imeweka jitihada nyingi katika kuhakikisha maadili yanazingatiwa, moja ya jitihada hizo ni programu ya maboresho ikiwemo ya utumishi wa umma na serikali za mitaa” aliongeza Mkuchika

Awali, Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu, Harold Nsekela alisema maadhimisho hayo husheherekewa kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Aidha, Jaji Nsekela alisema ni vyema watumishi wakatumia maadhimisho ya mwaka huu kujitafakari na kujipima utendaji wao na kujirekebisha pale wanapokosea.

Maadhimisho hayo hufanyika  Desemba 9 kila mwaka, lakini Tanzania ilisogeza mbele hadi Desemba 10 kupisha sherehe za uhuru ambazo hufanyika kila Desemba 9 nchini.