20
Mon, Jan
6 New Articles

Tume yaombwa kudumisha ushirikiano na Wadau

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Laurent Burilo akiongea na washiriki wa kikao kazi cha kujadili hali ya haki za binadamu na kuibua matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kwenye makundi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kilichofanyika Mkoani Morogoro, Oktoba 24—25, 2019.

News
Typography

Wadau wa haki za binadamu wameiomba Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora  kudumisha ushirikiano wa karibu na wadau wa taasisi zote ikiwemo za Serikali na Asasi za Kiraia ili kuendelea kujenga jamii  inayoheshimu na kuzingatia  haki za binadamu nchini.

 

Wadau walitoa ombi  hilo kwa wakati tofauti walipokuwa katika kikao kazi cha kujadili hali ya haki za binadamu na kuibua matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kwenye makundi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kilichofanyika Mkoani Morogoro, Oktoba 24—25, 2019.

Wakizungumza katika kikao hicho,  wadau hao walisema tume kuamua kuwa na ushirikiano na Asasi za Kiraia ni hatua nzuri katika  kuimarisha juhudi za pamoja za kusaidia jamii kutambua haki zao.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Josephine Lyengi alisema kuwa katika kikao hicho wamejifunza mengi kutoka kwa tume,na kuiomba  tume iendelee kushirikisha wadau katika kutekeleza majukumu yake kwani ushirikiano huo ukiimarika utasaidia sana jamii kutatua changamoto zao.

“Sisi kama serikali tunaipongeza tume kwa kazi nzuri inayofanya, na tupo tayari kupokea ushauri ili kujenga nchi yetu, sisi wote ni watanzania, hivyo hatuna budi kushirikiana katika kujenga nchi yetu”, alisema Lyengi

“Majukumu yetu yote tunayatekeleza kulingana na uwezo na rasilimali tulizonazo, hivyo serikali itaendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika na kutekeleza yale yote ambayo tunayaweza kulingana na uwezo wa rasilimali tulizonazo”, aliongeza

“Ushirikiano wowote unahitaji sana watu kujitolea ili kuweza kutimiza yale malengo tuliyojiwekea”, alisisitiza

Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Christopher Mushi alisema kuwa tume wanafanya vitu vinavyoenda  sambamba na juhudi ambazo wizara inafanya, hivyo aliwataka waendelee kujitoa na kushirikiana na wadau katika kuhudumia jamii.

“Safari tuliyoianza ya kuhudumia jamii bado ni ndefu, hivyo, hali na nguvu tuliyonayo tuendelee nayo, tushirikiane, hizi kazi tunazozifanya zitatoa muelekeo kwa jamii na kujenga ushawishi kwa Serikali”,alisema Mushi

 Marcela Rungu, mwakilishi Mtandao wa Wanawake (TGNP) alisema kuwa anaishukuru tume kwa kutambua mchango wa taasisi yao, na kuiomba tume kuendelea kushirikiana na TGNP.

‘Tunahitaji nguvu za pamoja katika kuendeleza juhudu hizi za kusaidia wananchi, tume mmefanya jambo zuri sana kuanzisha haya makundi ya kutetea haki za binadamu, tushirikiane kwa pamoja katika kuyaimarisha makundi haya ili yaweze kutoa matokeo tunayoyatarajia”, alisema Rungu

Kwa upande wa tume, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka, Germanus Joseph Kyafula aliwahakikishia wadau hao kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarika,na kuwaasa kuwa  wanapaswa kuendelea kushikamana ili kuleta mafanikio kwa taasisi zao na mafanikio ya nchi kwa ujumla.

Wadau hao walikutana Mkoani Morogoro kujadiliana hali ya haki za binadamu nchini na kuibua matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu  kwa lengo la kuandaa mpango kazi wa kushughulikia matukio hayo.

Itakumbukwa kuwa Julai, 2019 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) iliunda makundi mbalimbali ya haki za binadamu maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika maeneo wanayoyasimamia ili kusaidia kutatua changamoto za masuala ya haki za binadamu zinazoikabili jamii nchini.