20
Mon, Jan
6 New Articles

Makundi ya Haki za Binadamu yakutana kuandaa mpango kazi

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Josephine Lyengi akitoa mada katika kikao kazi cha kujadili hali halisi ya haki za binadamu nchini na kuibua matukio ambayo bado yanaonekana ni changamoto kubwa na kuyatengenezea mpango kazi wa kushughulikia. Kikao hicho kinafanyika Mkoani Morogoro kuanzia Oktoba 24—25, 2019.

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekutanisha makundi ya haki za binadamu iliyoyaunda ili kujadili hali ya haki za binadamu na kuibua matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kwenye makundi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu ili kuandalia mpango kazi wa kwenda kuyashughulikia.

 

Akieleza lengo la kikao kazi hicho cha siku mbili (2) kuanzia Oktoba 24—25, 2019 kinachofanyika Mkoani Morogoro, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Laurent Burilo aliwataka washiriki kutoka katika makundi hayo kutumia kikao hicho kujadili hali halisi ya haki za binadamu nchini na kuibua matukio ambayo bado yanaonekana ni changamoto kubwa na kuyatengenezea mpango kazi wa kushughulikia matukio hayo kwa lengo la kuyakomesha.

“Tumewakutanisha hapa ili mjadiliane na muibue matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu hususani katika maeneo hayo matatu na muandae mpango kazi utakaowasaidia kwenda kufanya ufuatiliaji na utafiti utakaosaidia mabadiliko ya sera nchini”, alisema Burilo

Kikao kazi hicho kimejumuisha wajumbe wa makundi ya haki za binadamu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Asasi za Kiraia,na  wawakilishi  kutoka Serikalini.

Itakumbukwa kuwa Julai, 2019 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) iliunda makundi mbalimbali ya haki za binadamu maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika maeneo wanayoyasimamia ili kusaidia kutatua changamoto za masuala ya haki za binadamu zinazoikabili jamii nchini.