11
Sat, Jul
7 New Articles

Wadau watakiwa kushirikiana kulinda haki za binadamu

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya(kulia) akimpokea na kumkaribisha Mgeni rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuwa anawasili katika kiwanja cha Nyerere Square jijini Dodoma kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika Disemba 10, 2018.

News
Typography

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya amewaomba wadau wa haki za binadamu kuungana na kushirikiana katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini.

Muya alitoa wito huo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika kiwanja cha Nyerere Square jijini Dodoma Desemba 10, 2018.

 

Akizungumza  katika maadhimisho hayo, Muya alisema kuwa haki za binadamu ni lazima ziheshimiwe na kila mmoja wetu kwa kuwa hazigawanyiki, hazitenganishwi na hazitofautiani kwa binadamu wote.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda haki ya mtu mwingine bila ubaguzi wowote wa utaifa, kijinsia, kabila,dini ama rangi ya mtu”, alisisitiza Muya

“Hivyo natoa wito kwa asasi za kiraia, washirika wa maendeleo, taasisi za dini na wadau wote wa haki za binadamu kuungana ili kulinda na kukuza haki za binadamu nchini”,alisema Muya

Muya aliongeza kwa kusema kuwa Tanzania kutambua na kuheshimu haki za binadamu kikatiba ni kielelezo cha kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia, usawa na kupinga ubaguzi wa namna yeyote na kuzuia ukatili hasa kwa makundi maalumu wakiwemo wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na wazee.

Alisema pamoja na kuadhimisha miaka sabini (70) ya  tamko la haki za binadamu, Tanzania inashiriki maadhimisho haya kwa lengo la kuikumbusha jamii kukuza na kulinda haki za binadamu na wajibu kama zinavyotamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria mbalimbali za nchi pamoja na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda.

Pia aliwakumbusha waajiri na wamiliki wa Viwanda kuwa wakati Tanzania inaelekea kujenga uchumi wa kati ni vyema wakazingatia haki za msingi za binadamu kwa wafanyakazi wao ikiwemo haki ya kuwapatia ujira wao kwa wakati na matibabu .

Awali,  Mgeni rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alisema kuwa  tangu awali serikali ya awamu ya tano lengo lake lilikuwa kutunza maadili na kulinda haki za binadamu jambo ambalo wamelifanya kwa nguvu kubwa.

“Leo tunashuhudia utoaji wa huduma kwa jamii umeimarika sana, nidhamu ya watumishi imekuwa kubwa hii ni kutokana  na usimamiaji wa nidhamu ya kazi na tutaendelea kuchukua hatua ili kulinda maadili na haki za binadamu”,alisema Majaliwa

Katika hatua nyingine alisema Serikali itaendelea kuhakikisha inaziwezesha taasisi zinazosimamia maadili na haki za binadamu ili ziweze kufanya kazi zake vizuri.