10
Fri, Jul
7 New Articles

Watanzania waombwa kuwa mabalozi wa haki za binadamu

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya akiongea katika kongamano la kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa lililofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jengo la Treasury Square jijini Dodoma Disemba 6, 2018.

News
Typography

Watanzania wameombwa kuwa mabalozi wa kulinda na kutetea haki za binadamu ili kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia haki za binadamu nchini.

Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya alipokuwa akizungumza katika kongamano la kuadhimisha  Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa lililofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jengo la Treasury Square jijini Dodoma Disemba 6, 2018.

 

Akiongea katika kongamano hilo, Muya alisema kuwa haki za binadamu ni suala mtambuka kwa kuwa linagusa nyanja zote hivyo ni jambo linalohitaji ushirikiano katika utekelezaji wake.

“Haki za binadamu ni suala mtambuka, naomba watanzania tuwe mabalozi na tushirikiane katika  kulinda na kutetea haki zabinadamu”, alisema Muya

“tunapoona haki za binadamu zinavunjwa popote pale tuwe na ujasiri wa kusimama na kutetea na kulinda haki hiyo”Muya alisisitiza

Muya akiongea kuhusu  kauli mbiu ya maadhimisho hayo ambayo ni udhibiti wa mgongano wa maslahi ndio nguzo muhimu ya kujenga utawala bora alisisitiza kuwa  ni muhimu kauli mbiu hiyo iendane na uzingatiaji wa dhana ya haki za binadamu.

“Tunaposhughulika na udhibiti wa mgongano wa  maslahi ni vyema  kuhakikisha kuwa unaendane  dhana ya haki za binadamu ili kujenga utamaduni wa jamii inayozingatia na kuheshimu haki na usawa”, aliongeza Muya

Kongamano hilo la siku moja ambalo kilele chake itakuwa Disemba 10, 2018 lilifunguliwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mohamed Chande na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya maadili na haki za binadamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, Asasi za Kiraia na taasisi za elimu.

Mwisho#