05
Fri, Jun
5 New Articles

Tume yatembelea ofisi za UN women

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya(kushoto) akiongea katika kikao kifupi kilichofanyika katika ofisi za shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala ya wanawake(UN women) jijini Dar es Salaam Novemba 21, 2018. Kulia ni anayeandika ni Mkuu wa kitengo cha Uongozi, ushirikishaji wa siasa na utawala cha UN women, Bi. Sara Negrao. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo.

News
Typography

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imefanya ziara katika ofisi za shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala ya wanawake(UN women) jijini Dar es Salaam Novemba 21, 2018.  

Akizungumza katika kikao kifupi na Mkuu wa kitengo cha Uongozi, ushirikishaji wa siasa na utawala cha UN women, Bi. Sara Negrao, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kufahamiana, kubadilishana uzoefu wa kazi na kuangalia uwezekano wa taasisi hizo mbili kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

 

Katika kikao hicho, Muya alitoa taarifa fupi kuhusu tume na majukumu yake, na aliendelea kuueleza uongozi wa shirika hilo kuwa pamoja na majukumu mengine iliyopewa kikatiba, Tume imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa uchaguzi mbalimbali katika mkoa wa Dar es Salaam.

Muya aliongeza kuwa Tume ingependa  kushirikiana na UN women katika shughuli mbalimbali inazozifanya hususani kufanya ufuatiliaji wa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020  ili kuongeza nguvu kwa pamoja na kufikia mikoa mingi zaidi.

Naye, Mkuu wa kitengo cha Uongozi, ushirikishaji wa siasa na utawala cha UN women, Bi. Sara Negrao baada ya kupata maelezo mafupi kutoka kwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, aliueleza ujumbe wa tume kuwa uwezekano wa kushirikiana upo ila ni vyema kuangalia  maeneo gani wanaweza kushirikiana.

Sara aliendelea kusema kuwa UN women imejikita katika kumjengea uwezo mwanamke ili aweze kujikomboa katika changamoto mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kisiasa.

Aliongeza kuwa katika uchaguzi ujao wamelenga kuangalia vitendo vya unyanyasaji na kuminywa kwa fursa za wanawake kushiriki katika shughuli za kisiasa.

“Vitendo vya unyanyasaji, ukatili na kuminywa kwa fursa za wanawake hususani katika kushiriki shughuli za kisiasa vimekuwa ni tatizo kubwa sana duniani”,alisema Sara

“Hivyo itakuwa vizuri kama tutaanza mapema kuangalia namna ya kushirikiana katika eneo hili na hata ikibidi kushirikisha wadau wengine ili kumsaidia mwanamke kuwa huru kushiriki vyema katika Nyanja ya siasa na shughuli nyingine za kiuchumi”, aliongeza

Kikao hicho kilimalizika kwa makubaliano kuwa wanaweza kushirikiana katika kazi mbalimbali na kwa kuanza wataangalia uwezekano wa  kushirikiana katika uchaguzi ujao.

Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya ilijumuisha Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo, Alexander Hassan, Afisa Uchunguzi, Mbaraka Kambona na Afisa Uchunguzi, Florence Chaki.