10
Fri, Jul
7 New Articles

NDI yaiahidi ushirikiano THBUB

News
Typography

Mkurugenzi Mkaazi wa taasisi ya kimataifa ya National Democratic Institute (NDI) nchini,  Sandy Quimbaya amekutana na uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo uwezekano wa kushirikiana katika kutoa elimu ya uraia kwa jamii na kufanya ufuatiliaji wa uchaguzi ujao nchini. 

 

Katika majadiliano hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za NDI zilizopo jijini Dar es Salaam, Septemba 20, 2018, Quimbaya aliueleza ujumbe huo wa tume kwa ufupi kuhusu majukumu ya NDI na kusema kuwa kulingana na upana na ukubwa wa majukumu waliyonayo tume ni wazi wangependa kushirikiana  nao. 

“Kulingana na upana wa majukumu ya tume tungependa kuona uwezekano wa hizi taasisi mbili  kushirikiana,”alisema Quimbaya

“Katika kufanikisha hilo mwezi Novemba NDI itaunda timu ya wataalamu itakayofanya mapitio na uchambuzi wa taarifa mbalimbali ikiwemo za tume na taasisi nyingine ili kubaini maeneo yenye changamoto, na katika kufanya hivyo watakuwa katika nafasi nzuri ya kuamua NDI na Tume wafanye ushirikiano katika maeneo gani,”aliongeza Quimbaya

Ujumbe wa Tume ulioongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya  ulitembelea ofisi za NDI zilizopo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na kujenga mazingira ya kushirikiana na taasisi hiyo ambayo imejikita katika kuimarisha misingi ya demokrasia duniani. 

Kwa upande wa tume,  Mkurugenzi wa Utawala Bora, Hajjat Fatuma Muya alieleza katika kikao hicho kuwa tume imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa uchaguzi lakini mara zote imekuwa inaishia kufanya ufuatiliaji huo hapa jijini Dar es Salaam kutokana na changamoto ya rasilimali fedha.

“Tume ingependa kuona inafanya ufuatiliaji wa uchaguzi  kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwa nchi nzima ili iwe katika nafasi nzuri ya  kuishauri serikali ipasavyo  kwa lengo la kuboresha uchaguzi wetu nchini” alisema Mkurugenzi huyo.

Muya aliongeza kwa kusema kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 vyama vya siasa hususan CCM, CUF na CHADEMA walikuwa na vikundi vyao vya ulinzi ambavyo vilikuwa vinajihusisha na ulinzi wakati wa kampeni jukumu ambalo kimsingi sio lao ni la jeshi la Polisi, Tume ililishughulikia kwa kuwasiliana na Tume ya Uchaguzi na liliweza kufanyiwa kazi na Serikali.

Aidha, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka Tume,  Alexander Hassan alieleza kikao hicho umuhimu wa kufanya mashirikiano katika kutoa elimu ya uraia kwa jamii kwani uzoefu katika uchaguzi mkuu uliopita na hata  uchaguzi mdogo unaoendelea  mwitikio wa jamii katika kushiriki uchaguzi umekuwa mdogo sana.

“Kama tutafanikiwa kuingia makubaliano ni vyema tukaanza na elimu ya uraia kwanza halafu ufuatiliaji wa uchaguzi ufuatie kwa sababu kwa hali ilivyo sasa uelewa na mwamko wa jamii kushiriki katika uchaguzi upo chini sana”alisema Alexander

“Hivi karibuni tume ilitiliana saini na Asasi za Kiraia thelathini (30) kwa lengo la kushirikiana katika kuelimisha jamii masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora, hivyo  tukifanikiwa kufanya ushirikiano katika hili tutawatumia hawa wenzetu kueneza elimu hii”, aliongeza.

Ujumbe wa tume ulikuwa na jumla ya watu wanne (4) ambao ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala Bora wa tume, Hajjat Fatuma Muya,   Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka Tume,  Alexander Hassan, Afisa Mwandamizi, Vicent Mbombo, na Afisa Mawasiliano Mbaraka Kambona.

NDI ni taasisi ya kimataifa kutoka Marekani inayojushughulisha na kuimarisha demokrasia katika nyanja tofauti tofauti  na pia misingi ya utawala bora.  

 Mwisho.