05
Fri, Jun
5 New Articles

Tume Yaombwa Kushiriki Mapambano Mimba za Utotoni

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo wa Tume, Alexander S. Hassan akizungumza wakati wa mafunzo ya mradi wa kuboresha upatikanaji wa haki kwa wote yaliyofanyika Mkoani Lindi Januari 7-11,2019. Kulia ni Afisa Mfawidhi kutoka Tume kanda ya kusini, Noel Chiponde na kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoani Lindi, Dk Bora Haule.

News
Typography

Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali watu Mkoani Lindi, Dk Bora Haule ameiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB) kushirikiana na Mkoa wa Lindi katika kampeni ya kupambana na mimba za utotoni.

Dk Haule, ambaye alikuwa anamuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, alitoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo ya kuboresha upatikanaji wa haki kwa wote yaliyohusisha watumishi wa serikali za mitaa na halmashauri yaliyofanyika mkoani Lindi januari 7-11,2019.

Dk Haule alisema kuwa takwimu za mwaka jana 2018 katika mkoa huo zinaonesha kuwa   wanafunzi wa
kike wapatao 137 wa kidato cha nne walipata ujauzito na kuacha shule.

Kufuatia changamoto hiyo, Dk Haule alisema kuwa mkoa umeamua kufanya kampeni maalum ya kupambana na tatizo la mimba za utotoni na kwa kuanzia wataandaa tamasha la ufukweni mapema mwaka huu kuhamasisha mtoto wa kike kusoma na kujihepusha na vitendo vinavyoweza kumfanya asiendelee na masomo.

"Hivyo tunaiomba tume iweze kushirikiana nasi katika tamasha tutakaloliandaa ili kumuwezesha na kumuelimisha umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu", alisema Dk Bora.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo wa Tume, Alexander S. Hassan aliupongeza mkoa kwa maamuzi ya kuanzisha kampeni hiyo ya kupambana na mimba za utotoni kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kama sio kuondoa kabisa mimba kwa watoto.

Katika hatua nyingine, Dk Haule aliwataka Watumishi wa Mamlaka za serikali za mitaa mkoani Lindi kusimamia haki za binadamu na upatikanaji wa haki za kisheria kwa wananchi wanao wahudumia.

Dk Haule alisema kuwa katika jamii kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na upatikanaji wa haki kisheria kutokana na wananchi kutojua haki zao na wapi wanaweza kwenda kuzidai endapo zitakiukwa.

Mafunzo hayo yaliyohusisha wakuu wa Idara kutoka halmashauri na  wakuu wa vitengo wa sekretarieti ya mkoa yameandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa lengo la kuwafundisha watumishi hao kwa kuwa ndio wanaowahudumia wananchi moja kwa moja.